Showing posts with label Mbinu mpya za ujenzi. Show all posts
Showing posts with label Mbinu mpya za ujenzi. Show all posts

Wednesday, April 4, 2018

NJIA RAHISI YA KUHAKIKI UBORA WA SARUJI UKIWA SITE:



Saruji hutumika sana katika ujenzi. Uimara wake hutegemea mambo mengi ikiwemo ubora wake.
Hivyo ni wazi kwamba ni muhimu kuchunguza ubora wa saruji kabla ya kuitumia.
Tumia njia zifuatazo kuchunguza ubora wa saruji yako.




1. TAREHE YA PAKEJI/KIFUNGASHIO:
Ubora wa saruji hupungua kadiri muda ilipotengenezwa na kupakiwa kwenye vifungashio unavyoongezeka.Saruji hupaswa kutumika siku 90 tangu kuwekwa kwenye kifungashio(kutengenezwa. Tazama tarehe ya kufungashwa kuhakiki kabla ya kuitumia


2. RANGI YA SARUJI:
Saruji iliyo kwenye ubora ina rangi ya kufanana (Uniform colour).Inakuwa na rangi ya kijivu



3. CHUNGUZA MABONGE:
Saruji haipaswi kuwa na mabonge kabla ya kutumika hivyo ikiwa na mabonde,ubora wake ni mdogo



4. JARIBU KWA KUSUGUA KATI YA VIDOLE:
Chukua saruji kidogo kati ya vidole vya mikono yako,sugua.
Ni lazima iwe laini,kama si laini,ubora wake ni hafifu



5 JOTORIDI:
Ingiza mikono yako ndani ya mfuko wa saruji.Inapaswa iwe na ubaridi.Ikiwa ya joto basi ubora si uliotakiwa



6. JARIBIO LA KUZAMISHA KWENYE MAJI:
Chukua kiasi kidogo cha saruji,kasha weka kwenye maji safi.Saruji yenye ubora huelea kwa muda kabla ya kuzama.


7. JARIBIO KWA KUGANDISHA:
Chukua kiasi cha saruji iliyochanganywa na maji,kasha weka kwenye maji kwa saa 24, ni lazima iwe imekauka na isiwe na nyufa

Tuesday, April 3, 2018

NYUFA/KREKI(CRACKS)



Nyufa hutokea zaidi kwenye nyumba zilizojengwa kwa tofali za saruji ama za udongo.
Mara nyingi sababu kuu ya kutokea nyufa kwenye nyumba ni kuzama ama kutitia kwa msingi wa nyumba/kipande cha msingi wa nyumba kuzama.




Kutitia/kuzama/kuhama kwa msingi wakati Fulani hutarajiwa,lakini unapozama kwa kiasi kikubwa huleta tatizo kubwa zaidi.

Kutitia kwa msingi hutokana na udongo kutohimili uzito wa nyumba. Ndio maana kuna umuhimu mkubwa wa kutumia wataalam katika ujenzi, ambao hutazama aina ya udongo na kutafuta namna ya kuzuia athari ya kutitia kwa msingi/nyumba kutokea.


Kutokea kwa nyufa,athari yake inaweza isionekane kwa muda mrefu kutegemea aina ya udongo unaobeba nyumba.


Kuziba nyufa si kazi ngumu,kazi ngumu ni kuzifanya zisijirudie.Watu wengi hutilia mkazo katika kuziba nyufa,badala ya kutilia mkazo katika kudhibiti kisababishi.



Zipo nyufa ambazo huzibwa na kujirudia.Mafundi wengi hupata lawama,kuziba na baada ya muda mfupi hujitokeza tena.


Wakati Fulani,nyufa huendelea kutokea kutokana na kuendelea kuzama taratibu kwa kipande /msingi.Ni muhimu kufanya jaribio kujiridhisha kama nyufa unayoziba inajirudia kutokana na kuendelea kuzama kwa msingi.



UNAFANYAJE KUJUA
Ziba vema nyufa,kisha kaa mwezi mmoja mpaka miwili. Tazama kama imejirudia.

Iwapo imejirudia na uliiziba kwa kufuata kanuni za kuziba nyufa,basi inatokana na kuendelea kuzama kwa msingi hasa sehemu yenye udhaifu wa udongo.


UNAZIBAJE KREKI?NYUFA


1.Undoa udongo wote wa zamani uliotumika kuunganisha tofali zako(mortar).Ondoa kwa makini na usiache kipande chochote chenye udhaifu.


2.Safisha vizuri sehemu uliyoondoa udongo,ondoa vumbi


3.Iwapo ufa ni mkubwa,unaweza kuweka vipande vya wavu/chuma.Ni muhimu kuhakikisha kwamba chuma /wavu unaoweka unakaa vema .Hakikisha pia wavu haichukui nafasi kubwa.
Ipo njia ya kutumia vipande vya gunia na zingine kadiri ya uzoefu wa mafundi.


4.Weka kiasi cha kutosha cha niru(grout).Ni vema kutumia niru ya vinyl(vinyl grout) kwa sababu ina uwezo wa kuhimili kutanuka na kusinyaa wakati wa joto/baridi.


5.Hatua kwa hatua weka mchanganyiko wako wenye urojo wa kutosha kuifanya sehemu iliyokuwa na mpasuko/ufa ivutie.


Zipo nyufa zitokanazo na kuharibika kwa tofali/tofali kuwa dhaifu.
tofali dhaifu husababisha nyufa



KWAKO FUNDI
Tushirikishe uzoefu wako katika kuziba nyufa/kreki.Tuambie hatua kwa hatua kadiri ya uzoefu wako.Tushirikishe kwa picha nyufa ulizokutana nazo.
Makala hii imeandaliwa na Pongu J-0765046644
Je Makala hii imekua msaada kwako? Kma ndio washirikisha wengine waweze kuelimika kwa kubonyeza share

Monday, March 26, 2018

KWA NINI NI MUHIMU KUZINGATIA PANDE ZA DUNIA UNAPOCHAGUA SEHEMU YA KUJENGA NA KUJENGA?




Kulingana na mapokeo na  utaalamu toka kale, ni muhimu sana kuzingatia pande za dunia unapotaka kujenga,hasa unapochagua sehemu ya kujenga.

Fuatana nami kupitia makala hii uelimike kuhusu uchaguzi wa eneo la kujenga
Picha ikionesha pande za dunia






UELEKEO WA KIWANJA (SITE ORIENTATION)

Uelekeo wa kiwanja maana yake ni mahali(nafasi) kilipo kiwanja kwa kuzingatia dira. Hutanabaishwa kwa kutazama upande wa mbele ya kiwanja chako unapotazama.Unaposimsms kwenye kiwanja chako na kutazama ilipo barabara, upande unaoutazama ndio uelekeo wa kiwanja chako.Kama kiwanja kina barabara upande wa kaskazini, basi uelekeo wako ni kaskazini(North facing site)

Kutokana na mapokeo  zipo pande nane ambazo huzingatiwa kulingana na lilipo jua.Pande hizi hutokana na pande nne kuu ambazo ni

  • Mashariki-Unatambulika ni upande ambao jua huchomoza

  • Magharibi-Unatambulika kuwa ni upande jua linapozama

  • Kaskazini-Unatazama mashariki,upande ulio kushoto kwako ni Kaskazini

  • Kusini-Utazamapo mashariki,upande uliopo kulia kwako ni kusini

Kona ambazo pande mbili kati ya pande kuu nne zilizotajwa hukutana,ni muhimu kwa sababu kani ya mvutano toka pande kuu nne huungana.

  • Kaskazini mashariki-Ni upande ambao pande mbili za kaskazini na mashariki zinakutana Kaskazini Magharibi-Ni upande ambao pande mbili za kaskazini na magharibi zinakutana

  • Kusini Magharibi-Ni upande ambao pande mbili za kusini na magharibi zinakutana

  • Kusini Mashariki-Ni upande ambao pande mbili za kusini na mashariki zinakutana




KWA NINI MWELEKEO WA KIWANJA NI MUHIMU SANA WAKATI WA KUCHAGUA KIWANJA CHAKO?

Jua ni muhimu sana katika maisha ya viumbe hai.
Jua husababisha mimea kujitengenezea chakula chake,ambayo baadae wanadamu hula.Jua husaidia mwili wa binadamu kutengeneza Vitamini D.Jua pia huleta nuru.Kwa kifupi ni vigumu kutofautisha jua na uhai wa viumbe.Ukiachilia mbali faida za jua,pia zipo hasara kwa viumbe,akiwwemo binadamu

Hivyo ni muhimu wakati  wa kupangilia nyumba, ni muhimu kuhakikisha binadamu anahakikishiwa miale ya jua yenye faida na kukingwa na miele mikali ya jua yenye madhara.Vymba na nafasi zote zinazohitajika kwenye nyumba ni lazima zipangiliwe kuhakikisha zinapata mwanga wa jua wenye faida na kukingwa na miale yenye kuleta athari
Mwelekeo wa nyumba yako kuzingatia mawio na machweo ya jua ni muhimu


JE NI UPANDE UPI MZURI KWA KIWANJA CHAKO?

Pande zote zinafaa,zikiwa zina faida na hasara yake.Mpangilio wa mji huzingatia uwepo wa barabara katika pande zote za mtaa(Kwa maeneo yaliyopangiliwa tu) na pande zote huhitajika kuwepo majengo(nyumba) ili kufanya mtaa(mji) uvutie na kufikika kwa urahisi

KIWANJA KINACHOTAZAMA MASHARIKI

Upande huu ndipo jua linapochomoza.Miale yenye faida huwa jua linapochomoza.Utafiti unaonesha jua la majira ya saa nne(asubuhi) husaidia mwili kuzalisha vitamin D.Hivyo kiwanja kitazamacho upande huu hutoa nafasi nzuri zaidi kupangilia nafasi zako katika nyumba,hasa ikitazama upande huu. Ukiamka unakutana na mwanga wa jua unaochochea ubongo kufanya kazi vema.Katika baadhi ya tamaduni upande huu huhusishwa na ucha Mungu, uaminifu, elimu na ibada.

UPANDE WA KASKAZINI

Upande huu una uhusiano mzuri na kuvuma kwa upepo na miale ya jua.Katika imani mbalimbali kiwanja kitazamacho Kaskazini huhusiana na nguvu na utawala

UPANDE WA KUSINI

Mara nyingi viwanja vyeye kutazama upande huu havipendelewi sana kwa sababu huhitaji zaidi umakini katika kupangilia nyumba yako na mazingira yanayohusiana na nyumba yako.Viwanja hivi hufaa zaidi kwa matumizi ya biashara kuliko ya makazi.

UPANDE WA MAGHARIBI

Ni upande jua linapozama.        

Ni muhimu kuwa makini unapopangilia nyumba yako kwa kiwanja kitazamacho upande huu

Je Makala hii imekusaidia kujifunza chochote?Kama ndio washirikishe wengine waelimike.
Usisite kuniandikia maoni yako na maswali kuhusu ujenzi.

Sunday, March 25, 2018

MAMBO YA MUHIMU KUZINGATIA UNAPOBUNI NA KUJENGA NYUMBA



1.MLANGO MKUBWA WA KUINGIA NDANI(MAIN DOOR)
picha kwa hisani ya Pongu J

Mlango mkuu wa kuingia kwenye nyumba ndio unaokaribisha anayeingia ndani.Kiimani ni lango la kukaribisha nguvu zote zenye faida na zenye madhara.Pia ni mlango mkuu wa kutoka ndani ya nyumba.
·         Ni muhimu mlango wa kuingia ndani uoane ama uwe katika uelekeo mmoja na lango kuu la kuingia (Gate)

·         Lango kuu(gate)  na mlango wa kuingia ndani ni vema view upande mmoja. Sababu kubwa ni kufanya kuwa na urahisi kuingia lango kuu na kutembea moja kwa moja kwenda kwenye mlango wa nyumba pasipo kuzinguka.Pia ni rahisi kujua anayeingia na kutoka
·         Mlango mkuu wa kuingia ni muhimu uwe mkubwa na iwe miwili(double door) yaani ufunguke sehemu mbili.

Pia ni muhimu nyumba kuwa na milango miwili ya nje kuruhusu kuingia na kutoka kwa urahisi pale inapohitajika, na kufanya hewa kuingia na kutoka na kuufanya mzunguko wa hewa ndani ya nyumba

·         Upande wa kuingia unapaswa kuwa mkubwa kuliko wa kutoka.Sababu kubwa ni kwamba,hapa ndipo hewa(air) inavuma kutoka nje kwenda ndani.Unapaswa iignie kwa wingi na kutoka kidogo kufanya nyumba ipumue(hewa izingike vema kwenye nafasi zote
·         Mlango wa kuingia unapaswa kuwa mkubwa kuliko yote kwenye nyumba.Sababu kubwa ni kuruhusu vitu kuingia na kutoka kama samani na vifaa vingine vikubwaPia nguvu huingia kupitia hapa,hivyo ni muhimu kuingia kwa wingi.

·         Ni muhimu mlango huu wa kuingia ufungukie ndani na kwa mzunguko wa akrabu (clockwise).Sababu kubwa ni kwamba inasaidia kuingia kwa urahisi kwa kusukuma.Pia ni rahisi ukiwa ndani unafungua kwa kutumia mkono wa kushoto na kuwa rahisi kukaribisha ama kuwa tayari kupokea kwa mkono wa kulia.

·         Mlango mkuu unapaswa kuwa na kizingiti.Epuka kuweka viatu mbele ya mlango wa kuingia ndani ya nyumba,sababu ni kuzuia wadudu na wanyama kuingia. Viatu huweza kuvuta wadudu kama nzi, na huweza kusababisha kujikwaa.Pia huleta picha mbaya mbele ya nyumba
·         Mlango mkuu ni muhimu uwe juu kutoka usawa wa ardhi, na kuufikia panapaswa kuwa na ngazi chache kuufikia na zinapaswa kuwa na idadi ya namba witiri. Sababu ya msingi ni kuzuia maji na wanyama wanaotambaa kufikia kirahisi.Pia kuwa juu kutoka usawa wa ardhi kunasababisha taka kutoingia ndani.

Sababu kwa nini ni muhimu kuwa na ngazi chache ambazo idadi yake ni witiri ni kwa sababu watu wengi hutumia mkono wa kulia,huanza kupanda ngazi kwa kunyanya kwanza mguu wa kulia,hivyo anapopanda atamaliza kwa kufika na mguu wa kulia.

·         Mlango mkuu unapaswa kuonekana kwa urahisi na uvutie.Sababu ni kwamba mgeni anapofika anapaswa kuuona kwa urahisi na umvutie(usiwe gizani na usiwe mweusi)
·         Mlango uwe unavutia na ubunifu wa kutosha ikiwemo picha ama alama zenye kuvutia.Bianadamu hupenda kuona vitu vyenye kuvutia

·         Mlango unapaswa utengenezwe zaidi kwa kutumia mbao kwa sababu mbao hudumu nan i rahisi kuweka nakshi na urembo

**ZINGATIA-Mbao inayotumika kutengeneza mlango isitokane na miti isiyokomaa,sitokane na miti inayotoa maua mazuri ya biashara wala harufu kali na isitokane na miti ambayo ipo hatarini kutoweka ili kuzuia upotevu wa miti yenye faida zaidi kwa matunda,maua na yenye historia.
Picha kwa hisani ya mtandao



JE NI MAMBO GANI UNAPASWA KUYAEPUKA UNAPOBUNI MLANGO MKUBWA WA KUINGIA NDANI (AMA KUJENGA)
1.       Kwa nyumba za kuishi epuka mlango wenye kuzunguka (circular door) nay a kutembea (sliding door) kwa sababu kubwa ni kwamba haitoi urahisi katika kutumia na haidumu

2.       Epuka mlango wako mkubwa kuingia kwenye nyumba kutazamana moja kwa moja na mlango mkuu wa nyumba nyingine.Pia mlango usitazamane na msikiti,kanisa ama mahakama. Unapofungua mlango wa nyumba yako mtu huweza kutazama moja kwa moja ndani

3.       Epuka kuwa na miti mikubwa ama kitu kisichohamishika mbele ya mlango wako,utakuzuia kuonavitu vilivyo mbele ya mlango na kisaikolojia  usababisha pingamizi ama vizuizi.

4.       Epuka mlango kutazama moja kwa moja gofu/magofu,unapofungua asubuhi utatazama gofu

5.       Epuka kujenga tanki chini(underground tank) ama tanki la maji taka mbele ya mlango wa kuingia.iwapo itahitajika kusafisha ama kufanya marekebisho itasumbua kupita

6.       Epuka kuweka mlango wa kuingia ndanin ya nyumba kwenye kona ya nyumba.Ni vigumu kupangilia samani kwa sababu kona itatumika kwa ajili ya nafasi ya kutembea.

7.       Epuka kuwa na ukuta unapofungua tu mlango wa kuingia, hewa na mwanga utazuiliwa kupita

8.       Epuka mlango unaojifunga wenyewe. Endapo patakuwa na upepo mkubwa mlango unaweza kujifunga huku funguo zikiwa ndani.

9.       Epuka mlango uliochakaa na unaotoa kelele unapofunguliwa/kufungwa-unaonesha udhaifu wa mlango, uzembe

Je, makala hii imekusaidia kwa njia yoyote? Kama ndio usisite kuwashirikisha wengine kusoma waelimike.
Kwa maswali kuhusu ujenzi usisite kuwasiliana nami
PONGU J- +255 765046644

Sunday, March 11, 2018

DONDOO MUHIMU KATIKA UCHAGUZI WA KIWANJA CHA KUJENGA NYUMBA YAKO YA KUISHI



Kutafuta kiwanja ni hatua ya awali kabisa kuelekea kujenga nyumba ya ndoto yako. Hatua hii ni muhimu sana kwani ardhi ni gharama na ukishajenga, kubadili maamuzi huleta gharama kubwa zaidi.
Fuatana nami katika makala hii ili uweze kufuhamu ni mambo gani muhimu katika uchaguzi wa kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi.
Kwa kifupi, nyumba ya kuishi inapaswa kuwa ni sehemu yenye utulivu , amani, uoto mzuri na ijengwe  sehemu yenye urahisi wa upatikanaji wa huduma muhimu kama maji,usafiri na yenye kuleta msawazo wa mawazo. Pia kila binadamu hupenda amani  ,hivyo ni muhimu uchaguzi wa kiwanja uzingatie dhana hii.
Yafuatayo ni mambo ya msingi unayopaswa kutilia mkazo unapochagua eneo la kujenga




1.      Imani yako kwanza ni muhimu. Inashauriwa usimame kwenye eneo unalotaka kununua ksha sikiliza mvuto wa eneo hilo.Kama panakuvutia moyo wako utakuvutiwa nalo,kama hapana,utakuwa na mashaka nalo



2.      Chunguza historia ya eneo unalotaka kununua.
Unashauriwa kununua eneo lenye historia njema kwa jamii iliyopita kabla yako.Iwe ni sehemu ambayo watu walioishi walikuwa na furaha ,amani na umoja.Sababu kubwa ya kuchunguza ni kwamba kuna uhusiano mkubwa sana wa kimaendeleo kati ya watu walioishi awali na namna ardhi ilivyotumika.Kuishi sehemu yenye watu wenye amani,upendo na mshikamano kutakufanya wewe na kizazi chako uishi pia kwa amani ,upendo na mshikamano.
3.      Kiwanja ambacho kinafikika.
Kiwanja chenye barabara pande zote huhusiana na furaha, afya njema na mafanikio. Huwa na hewa, mwanga na nafasi ya kutosha
Kwa kiwanja kisichokuwa na barabara pande zote,ni muhimu kiwe na barabara kwa upande wa kaskazini ama Mashariki mwake.Sababu ya msingi ni ni kwamba nyumba itakayojengwa itakuwa na mwanga na hewa ya kutosha kuanzia asubuhi.
Katika sehemu za Asia hasa India,kiwanja chenye maji upande wa kaskazini ama mashariki hupendelewa zaidi,sababu ikiwa ni uwezekano mkubwa wa kuwepo mwanga,hewa na mandhari ya kutosha na kwamba miale ya jua ya asubuhi(Ultraviolet light ) husaidia kuua vijidudu kwenye maji na kuyafanya yafae kutumika
4.      Hakikisha eneo unalonunua ni la makazi ama makazi na biashara.
Itakufanya uepuke na usumbuufu kubomolewa ama kuwa na hofu ya kuhamishwa.Hakikisha unafuata taratibu zilizowekwa katika kumiliki ardhi.
Nyumba iliyozungukwa na maji upanse wa mashariki.Picha kwa msaada wa architectureideas.com

Je ni kiwanja cha namna gani hakikufai katika ujenzi wa makazi?
1.      Epuka kiwanja kinachouzwa na mtu aliyepatwa na dhiki/filisika
Kiwanja cha namna hii ni muhimu kinunuliwe kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia kumwinua mwenye dhiki ama shida.
Ununuzi wa kiwanja cha namna hii kwa malengo ya kujinufaisha wewe zaidi kitakufanya baadae ukose furaha na amani na labda manung’uniko yatokanayo na muuzaji ama jamii inayozunguka yanaweza kukuondolea heshima na utu.
2.      Epuka kiwanja kilicho jirani/kinachopakana  na maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya kijamii.
Maeneo haya ni kama kumbi za starehe, kanisa, msikiti , kiwanda, chuo, jeshini,  shule, soko, sehemu stesheni za magari.
Maeneo haya huwa na kelele nyingi  na mara nyingi matumizi ya maeneo haya huadhiri maeneo yaliyo jirani,ikiwemo kubadilishwa kwa matumizi wakati wowote.Ni vigumu kulea watoto na kuwakuza kimaadili katika maeneo yaliyojirani na sehemu nilizozitaja hapo juu.

3.      Epuka kununua eneo linalomilikiwa ama lililomilikiwa na taasisi za kiimani.
Wengi wanaweza wasielewe hili. Wakati wowote taasisi za kiimani huweza kuuza maeneo kwani  ni haki yao ya msingi. Lakini kadiri mahitaji yanapoongezeka miaka kwa miaka,uwezekano mkubwa wa kulihitaji eneo lao la awali hujitokeza.Kwa sababu ni vigumu kushindana na taasisi, ni ukweli usiopingika kwamba mazingira yatakufanya ulazimike kuondoka na kuanza maisha upya,licha ya kwamba utalipwa.
4.      Epuka eneo lililo jirani na sehemu za taka na zenye harufu kali.
Kiwanja chako hakipaswi kuwa jirani na machinjio, mashimo ya taka ngumu na maji taka, mitaro mikubwa ya maji, sehemu wanapotengeneza na kuuza viatu, tairi kwa wingi.
Meneo haya kwa wakati wote yanaweza yakawa na harufu kali na kufanya usiishi kwa furaha na amani.
5.      Epuka kununua kiwanja eneo lenye magofu mengi.
Zipo sehemu ambazo zina magofu mengi yatokanayo na sababu mbalimbali.Mara nyingi maeneo haya huwa ni kivutio cha vibaka, majambazi na wanyama wakali. Kuishi maeno haya huzua hofu.
eneo lenye magofu(picha kwa msaada wa mtandao)

6.      Epuka kiwanja kilichopo eneo lenye dungusi (kakati) (jamii ya mimea kama mpungate.
Sababu ya msingi ni kwamba maeneo yenye mimea hii huwa na udongo dhaifi usio rafiki kwa msingi wa nyumba yako.
7.      Epuka kiwanja  kilicho sehemu yenye mchwa na kumbikumbi wengi
Sababu kubwa ni kwamba ni vigumu kuyaondoa makazi ya mchwa. Mchwa huharibu mbao na hata kudhoofisha msingi na kuta za nyumba. Pia huweza kushambulia samani mbalimbali.
8.      Epuka kiwanja kidogo kilichozungukwa na viwanja vikubwa.
Sababu kubwa ni kwamba mmiliki wa kiwanja kidogo hulazimika kujenga nyumba ndogo ,na wamiliki wa viwanja vikubwa  hujenga nyumba kubwa na kuwa na matumizi mengi zaidi kwenye eneo moja, hivyo mmiliki wa nyumba ndogo (kiwanja kidogo)  hushawishika kujitazama kama mnyonge na mara nyingi hudhani anaonewa(inferiority complex)
9.      Epuka kiwanja chenye mapingamizi ya milima,mabonde na majengo marefu hasa upande wa mashariki na kaskazini mwa kiwanja.
Sababu  kubwa ni kwamba  majengo marefu na milima/mabonde huzuia hewa ya kutosha ,mwanga na huweka kivuli (giza) kwenye nyumba.
Habari njema ni kuwa kiwanja kilicho na milima ama majengo marefu upande wa kusini na upande wa magharibi husaidia kuzuia miale mikali ya mwanga.
10.  Epuka kiwanja kilicho na  nguzo kubwa za umeme kwenye kona ya kaskazini-mashariki.
Sababu kubwa ni kwamba umeme unaopita kwenye nguzo huwa na mawimbi (electrical waves) ambazo huwa na madhara na ukubwa wa nguzo huzuia mwanga na hewa kufikia nyumba itakayojengwa.
11.  Epuka kiwanja chenye nyufa/mipasuko(cracks) na udongo wenye mfinyanzi.
Nyufa kwenye ardhi huwa na uhusiano mkubwa na udongo wa mfinyanzi unaoruhusu maji mengi kutuama.Udongo huu si rafiki kwenye ujenzi na huhitaji gharama kubwa kujenga msingi.

12.  .Epuka kiwanja chenye miti mingi yenye mizizi mirefu na minene
Kama kiwanja unachotaka kujenga  ni kidogo na kina miti mingi yenye mizizi mikubwa na minene inayotambaa,si vema kukinunua kwa sababu mzizi hukua na kusababisha nyufa kwenye msingi na hata kufikia kuta za nyumba
13.  Epuka kiwanja kilichopo kwenye makutano ya barabara kuu hasa makutano yenye kutengeneza herufi T ama Y.
Kiwanja kilichopo kwenye makutano huwa na kelele nyingi, vumbi na wakati Fulani huondoa sitiri(privacy). Makutano yenye kutengeneza herufi T ama Y  kuielekea nyumba (kiwanja) ni rahisi kutokea ajali hasa kwa magari kugongana, watu kugongwa wakati wa kuvuka na pia heleta hofu ya kudhani gari zitagonga nyumba.
nyumba iliyojengwa kwenye kiwanja kilicho kwenye makutano ya barabara


14.  Epuka kiwanja chenye umbo la duara,sambusa ama pembetatu.
Kiwanja cha namna hii kama si kikubwa huongeza ugumu katika kuongeza matumizi na kujenga nyumba yenye ukubwa wa kutosha.Katika imani Fulani viwanja vyenye umbile la duara na pembetatu huhusianishwa na huzuni, umasikini na magonjwa.


Ahsante.
Makala imeandaliwa na Pongu J
+255 717 903089, +255 765046644



Sunday, July 19, 2015

KUKAMILISHA NDOTO YA NYUMBA YAKO

Picha ikionesha sehemu za ndani za nyumba kadiri ya muono wa msanifu-Imesanifiwa na P.J



Kila mtu anapotaka kujenga nyumba,huwa na picha ya nyumba aliyenayo.
Uzoefu wangu unaonesha kwamba watanzania wengi huwa hawana muono wa kitu wanachokitaka.Ukikutana na watu wengi wanaohitaji ramani ,huishia kufananisha maono yao na nyumba aliyeiona kwa nje,eitha ya jirani ama rafiki ama mtu maarufu.


Kwa kifupi ningepnda tushirikishane ujuzi kidogo.Ili kuitafsiri ndoto kuhusu kitu unachokitaka ni vizuri kutazama yafuatayo


1.Ukubwa-ukijumuisha,urefu,upana,ukubwa wa vyumba,idadi ya watu watakaotuia nyumba


2.Uhusiano kati ya nafasi moja na nyingine,ni vema picha ulionayo katika fikra zako iwe na tafsiri /picha ya jinsi sehemu moja na nyingine zinavyooana-mfano sebule na dining na vyumba n.k


3. Iwe na picha ya rangi utakazopiga ktka nyumba,kama ni rangi moja ijulikane,kama ni rangi tofauti ijulikane,kama ni aina ya texture ijulikane.Rangi pia ijumlishe ndani,nje,paa


4.Ndoto ni lazima iwe na picha ya jinsi madirisha,milango na vitu vingine vitakavyokuwa.Hii inajumuisha aina ya malighafi itakayotumika,rangi/texturena ukubwa

5.Ni vema ndoto ikawa na picha ya mazingira yanayokuzunguka.Kitu ukiwazacho moyoni mwako huwa.Jinsi unavyofikiri ndivyo unavyokuwa na mazingira huwa vile unavyoyatengeneza.Hivyo kabla ya kuanza kuamua kujenga ni muhimu ukawa na picha ya jinsi mazingira yatakayokuzunguka yatakavyokuwa.Utapaswa kujua bustani inayozunguka,maua,miti ,uoto wake kwa ujumla,majirani


6.Mwisho kabisa tafsiri ya ndoto yako iende kwenye gharama unayotaka kuitumia

Picha kwa hisani ya Pongu J

Nawasilisha na nakaribisha maoni.

Wednesday, July 8, 2015

UCHAGUZI WA RANGI KATIKA NYUMBA

Rangi katika nyumba ina faida kuu mbili,zikiwa ni kuongeza nakshi (kupendezesha ) na kazi ya pili ni kulinda kuta.

unaionaje rangi hii






picha zote ni mali ya Joseph P.

Rangi za kuta zinaweza kuwekwa katika makundi mawili ya rangi msingi na rangi sekondari (upili)
Rangi msingi ni rangi ambazo hupigwa ili kuwezesha rangi upili kudumu.Hujulikana kama primer kwa lugha ya kiingereza

Makala hii fupi inalenga kushirikisha wasomaji na wale ambao wangependa kujenga kuhusu uchaguzi wa rangi.

Ni wazi kuwa kila mtu ana uchaguzi wake wa rangi,na mara nyingi kuvutia kwa rangi ni baina ya mtazamaji na maono yake.

Zipo rangi zilizopoa na zinazong'aa sana.Ni sawa na kusema rangi zinazoakisi zaidi mwanga na zile za kutunza mwanga.

Ndugu msomaji ,nini maoni yako kuhusu rangi za kung'aa na rangi za kupoa.Je wewe binafsi unapenda nyumba yako iweje ukijenga.Kuanzia rangi ya paa mbaka kuta.Unapata picha gani unapofikiri kuhusu nyumba yako?

Niambie wewe umependa rangi ipi kati ya hizo juu.Una maoni gani kwa msanifu wa nyumba hizo hapo juu kuhusu rangi?
Tujadiliane

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WA NYUMBA ZETU!?


 Na Tumainiel W. Seria; Mkadiriaji Majenzi
“Nyumba bora, salama na nafuu ni hitaji muhimu kwa kila familia. Bila kuwa na mahali pazuri pa kuishi, watu hawataweza kuwa sehemu ya jamii inayozalisha, watoto hawataweza kujifunza na familia hazitastawi” anaeleza   Bw Tracy Kaufman, Mtafiti wa makazi nafuu kutoka Marekani (http://www.habitat.org/how/poverty.html)

Historia ya binaamu inaelezea mabadiliko makubwa ya ukuaji katika awamu tofauti tofauti za maisha yake.  Kutoka kutembea kwa kuinama mpaka kutembea wima. Kutoka kwenye ugunduzi wa moto, zana za mawe, magome ya miti kujisitiri maungo mpaka ugunduzi wa viatu, nguo, umeme, kompyuta na njia nyingi za usafiri bila kusahau bidhaa mbalimbali za kurahisisha kazi na kujenga makazi bora yenye kila aina ya madoido. 

Binadamu wa awali kabisa wanaelezwa kuwa na utaalamu wao ambao kutokana na hali halisi ya wakati huo ni wa kiwango duni sana kama utalinganishwa kwa nyakati za sasa. Binadamu wa kale alianza kuishi kwenye mapango na mahema ya miti, akitumia nyasi na ngozi za wanyama. Nyumba hizi hazikuwa na milango wala madirisha. Baadae akajua namna ya kutengeneza nyumba za miti na udongo, na baade wakatengeneza tofali za udongo za  kuchoma kwa joto la jua.

Makazi ya kale kwa maana ya nyumba za kuishi binadamu yalihusisha matumizi ya vitu asili moja kwa moja katika ujenzi wake tofauti na sasa ambapo bidhaa ya asili inasanisiwa kupata bidhaa nyingine katika hali ya kuongeza ubora na umaridadi. Nyumba iliyokuwa maalumu kwa mifugo haikuwa tofauti sana na anayoishi binadamu na wakati mwingine ilikuwa inatengenezwa kuwezesha mifugo kama ng’ombe, kondoo na mbuzi kuishi mahali pamoja na binadamu. Wataalamu wa historia wanatueleza kuwa nyumba nyingi za kale zilijengwa kutegemeana na tamaduni na mila za jamii husika.

Kwa kadiri miaka inavyokwenda binadamu amezidi kuwa mgunduzi wa bidhaa na mbinu mbalimbali zitakazomuwezesha kukabiliana na mazingira yanayomzunguka. Ugunduzi huo unahusisha ujenzi wa nyumba bora na bidhaa zake zinazoikidhi mahitaji muhimu kumuwezesha binadamu kuishi mahali safi salama huku kukiwa na nyongeza ya urembo na umaridadi wa aina tofauti tofauti. 

Nikukaribishe katika mfululizo wa makala hii itakayohusu kuwajua wataalamu mbalimbali katika taaluma ya ujenzi, hususani ujenzi wa nyumba za kuishi binadamu sambamba na umuhimu wa mjenzi kuwashirikisha watalamu hao katika kila hatua ya ujenzi wake kwa minajili ya kupata nyumba iliyobora, nzuri, salama na yenyekukidhi mahitaji. 

Nakumbuka wakati fulani nikiwa mwanafunzi Chuo Kikuu (UCLAS) mwalimu wangu wa somo la Ujenzi alipata kuniambia tukiwa mapumziko ya chakula kuwa kila mtu ni mbumbumbu kwa jambo fulani bila kujali vyeti alivyonavyo; akimaanisha kuwa kama wewe ni mtaalamu katika taaluma fulani uliyosomea ama kujifunza lazima utakuwa mbumbumbu kwenye taaluma nyingine ambazo hujajifunza. Akadai kuwa kadiri mtu anavyozidi kusoma jambo moja kwa undani zaidi ndivyo anavyozidi kuacha mambo mengine mengi na kubobea kwenye hilo moja pekee. Daktari aliyebobea kwenye upasuaji mkubwa kwa mfano, hawezi kuwa mjuzi kwa kiwango kile kile sawa na mtu mwingine anayeshugulika na maswala ya umeme kama taaluma yake.

Binadamu wa sasa anajipenda mno na anatamani kufaidi maisha yake kwa kadiri awezavyo. Moja ya matamanio hayo ni makazi bora yatakayompendeza kutegemeana na uwezo wake kifedha na kiutaalamu kugharamia hilo.

Lakini wapo watu wengi ambao wanatamani kuwa na makazi yanayokonga roho zao bila kujali kama wana uwezo mkubwa kifedha kugharamia umaridadi wanaoutaka ama la na wapo wengine ambao wao hujenga tu kwasababu inawalazimu wajisitiri ndani ya jengo wasidhurike na mashambulizi ya wanyama wakali na ama hali ya hewa ya kidunia. 

Hawa wanaojenga tu alimradi ni jengo la wao kuishi husababishwa kuamua hivyo ama kwa kutokujua wapi na ni nani wamuone kwa ushauri na pia uwezo mdogo kiuchumi. Baadhi pia hujenga kwa mazoea na hata mafundi wanaowatumia sehemu kubwa wanatumia uzoefu pekee.

Nyumba iliyojengwa kwa gharama kubwa sio lazima iwe nyumba bora. Kwa tafsiri rahisi nyumba bora ni ile inayokidhi mahitaji muhimu ya binadamu kuishi ndani na kujisitiri kwa usalama bila kupata madhara. Hii ni pamoja na mazingira yaliyoizunguka nyumba hiyo. Tutaona baadae mahitaji hayo muhimu ni yapi. Kwasasa itoshe kufahamu kuwa gharama zilizotumika kujenga makazi yetu ya uswahilini zinatosha kabisa kujenga makazi bora zaidi kwa kuhusisha wataalamu na kuacha kujenga kwa mazoea, sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo kiuchumi na kuogopa kuwashirikisha wataalamu kwa kuhofia gharama.

Leo ikiwa ni sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hii tutaangalia kwa ukaribu zaidi dhana nzima ya nyumba bora ya binadamu ambapo madhumuni na miundo yake hutegemeana sana na hali halisi ya kidunia kwa utofauti wa sehemu moja na nyingine. Hii ni dhana tata kidogo.

Dhumuni kubwa la kuwa na nyumba ya kuishi ni kumpatia mwanadamu usiri wa mambo yake binafsi, na kumlinda dhidi ya madhara yatokananyo na hali ya hewa ya kidunia na viumbe wengine hatari kwa binadamu. Malengo mengine ni raha, ufariji na mahali pa kuendeleza uzao na kutunza afya ya mwanadamu. Nyumba ya kuishi inajitofautisha sana na mejengo mengine kama ya biashara, ofisi, masoko, hospitali, viwanda n.k. Tofauti hiyo hutegemeana sana na lengo la matumizi ya jengo husika kama nilivyoeleza hapo juu.

Ili jamii iweze kuwa na makazi bora inalazimu timu ya wataalamu mbalimbali washirikiane kwa ukaribu sana ili kufanikisha hilo. Makazi bora lazima yahusishe nyumba bora na miundombinu inayoizunguka. 

Watu wengi wanaamini kujenga nyumba ya kuishi ni jambo gumu sana katika maisha yetu na hivyo kuishia kujenga alimradi tu ni kijumba cha kujisitiri. Ni kweli ujenzi ni gharama, lakini ukiwa na mipango mizuri na malengo thabiti unaweza kufanikisha kuwa na nyumba yako iliyo bora kwa urahisi kabisa. Kila kinachopangwa kikapangika vizuri huleta matokeo mazuri. 

Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya mambo muhimu yanayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.

Makala  hii kwa hisani ya Ujenzibongo blog