Sunday, March 11, 2018

DONDOO MUHIMU KATIKA UCHAGUZI WA KIWANJA CHA KUJENGA NYUMBA YAKO YA KUISHI



Kutafuta kiwanja ni hatua ya awali kabisa kuelekea kujenga nyumba ya ndoto yako. Hatua hii ni muhimu sana kwani ardhi ni gharama na ukishajenga, kubadili maamuzi huleta gharama kubwa zaidi.
Fuatana nami katika makala hii ili uweze kufuhamu ni mambo gani muhimu katika uchaguzi wa kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba ya makazi.
Kwa kifupi, nyumba ya kuishi inapaswa kuwa ni sehemu yenye utulivu , amani, uoto mzuri na ijengwe  sehemu yenye urahisi wa upatikanaji wa huduma muhimu kama maji,usafiri na yenye kuleta msawazo wa mawazo. Pia kila binadamu hupenda amani  ,hivyo ni muhimu uchaguzi wa kiwanja uzingatie dhana hii.
Yafuatayo ni mambo ya msingi unayopaswa kutilia mkazo unapochagua eneo la kujenga




1.      Imani yako kwanza ni muhimu. Inashauriwa usimame kwenye eneo unalotaka kununua ksha sikiliza mvuto wa eneo hilo.Kama panakuvutia moyo wako utakuvutiwa nalo,kama hapana,utakuwa na mashaka nalo



2.      Chunguza historia ya eneo unalotaka kununua.
Unashauriwa kununua eneo lenye historia njema kwa jamii iliyopita kabla yako.Iwe ni sehemu ambayo watu walioishi walikuwa na furaha ,amani na umoja.Sababu kubwa ya kuchunguza ni kwamba kuna uhusiano mkubwa sana wa kimaendeleo kati ya watu walioishi awali na namna ardhi ilivyotumika.Kuishi sehemu yenye watu wenye amani,upendo na mshikamano kutakufanya wewe na kizazi chako uishi pia kwa amani ,upendo na mshikamano.
3.      Kiwanja ambacho kinafikika.
Kiwanja chenye barabara pande zote huhusiana na furaha, afya njema na mafanikio. Huwa na hewa, mwanga na nafasi ya kutosha
Kwa kiwanja kisichokuwa na barabara pande zote,ni muhimu kiwe na barabara kwa upande wa kaskazini ama Mashariki mwake.Sababu ya msingi ni ni kwamba nyumba itakayojengwa itakuwa na mwanga na hewa ya kutosha kuanzia asubuhi.
Katika sehemu za Asia hasa India,kiwanja chenye maji upande wa kaskazini ama mashariki hupendelewa zaidi,sababu ikiwa ni uwezekano mkubwa wa kuwepo mwanga,hewa na mandhari ya kutosha na kwamba miale ya jua ya asubuhi(Ultraviolet light ) husaidia kuua vijidudu kwenye maji na kuyafanya yafae kutumika
4.      Hakikisha eneo unalonunua ni la makazi ama makazi na biashara.
Itakufanya uepuke na usumbuufu kubomolewa ama kuwa na hofu ya kuhamishwa.Hakikisha unafuata taratibu zilizowekwa katika kumiliki ardhi.
Nyumba iliyozungukwa na maji upanse wa mashariki.Picha kwa msaada wa architectureideas.com

Je ni kiwanja cha namna gani hakikufai katika ujenzi wa makazi?
1.      Epuka kiwanja kinachouzwa na mtu aliyepatwa na dhiki/filisika
Kiwanja cha namna hii ni muhimu kinunuliwe kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia kumwinua mwenye dhiki ama shida.
Ununuzi wa kiwanja cha namna hii kwa malengo ya kujinufaisha wewe zaidi kitakufanya baadae ukose furaha na amani na labda manung’uniko yatokanayo na muuzaji ama jamii inayozunguka yanaweza kukuondolea heshima na utu.
2.      Epuka kiwanja kilicho jirani/kinachopakana  na maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya kijamii.
Maeneo haya ni kama kumbi za starehe, kanisa, msikiti , kiwanda, chuo, jeshini,  shule, soko, sehemu stesheni za magari.
Maeneo haya huwa na kelele nyingi  na mara nyingi matumizi ya maeneo haya huadhiri maeneo yaliyo jirani,ikiwemo kubadilishwa kwa matumizi wakati wowote.Ni vigumu kulea watoto na kuwakuza kimaadili katika maeneo yaliyojirani na sehemu nilizozitaja hapo juu.

3.      Epuka kununua eneo linalomilikiwa ama lililomilikiwa na taasisi za kiimani.
Wengi wanaweza wasielewe hili. Wakati wowote taasisi za kiimani huweza kuuza maeneo kwani  ni haki yao ya msingi. Lakini kadiri mahitaji yanapoongezeka miaka kwa miaka,uwezekano mkubwa wa kulihitaji eneo lao la awali hujitokeza.Kwa sababu ni vigumu kushindana na taasisi, ni ukweli usiopingika kwamba mazingira yatakufanya ulazimike kuondoka na kuanza maisha upya,licha ya kwamba utalipwa.
4.      Epuka eneo lililo jirani na sehemu za taka na zenye harufu kali.
Kiwanja chako hakipaswi kuwa jirani na machinjio, mashimo ya taka ngumu na maji taka, mitaro mikubwa ya maji, sehemu wanapotengeneza na kuuza viatu, tairi kwa wingi.
Meneo haya kwa wakati wote yanaweza yakawa na harufu kali na kufanya usiishi kwa furaha na amani.
5.      Epuka kununua kiwanja eneo lenye magofu mengi.
Zipo sehemu ambazo zina magofu mengi yatokanayo na sababu mbalimbali.Mara nyingi maeneo haya huwa ni kivutio cha vibaka, majambazi na wanyama wakali. Kuishi maeno haya huzua hofu.
eneo lenye magofu(picha kwa msaada wa mtandao)

6.      Epuka kiwanja kilichopo eneo lenye dungusi (kakati) (jamii ya mimea kama mpungate.
Sababu ya msingi ni kwamba maeneo yenye mimea hii huwa na udongo dhaifi usio rafiki kwa msingi wa nyumba yako.
7.      Epuka kiwanja  kilicho sehemu yenye mchwa na kumbikumbi wengi
Sababu kubwa ni kwamba ni vigumu kuyaondoa makazi ya mchwa. Mchwa huharibu mbao na hata kudhoofisha msingi na kuta za nyumba. Pia huweza kushambulia samani mbalimbali.
8.      Epuka kiwanja kidogo kilichozungukwa na viwanja vikubwa.
Sababu kubwa ni kwamba mmiliki wa kiwanja kidogo hulazimika kujenga nyumba ndogo ,na wamiliki wa viwanja vikubwa  hujenga nyumba kubwa na kuwa na matumizi mengi zaidi kwenye eneo moja, hivyo mmiliki wa nyumba ndogo (kiwanja kidogo)  hushawishika kujitazama kama mnyonge na mara nyingi hudhani anaonewa(inferiority complex)
9.      Epuka kiwanja chenye mapingamizi ya milima,mabonde na majengo marefu hasa upande wa mashariki na kaskazini mwa kiwanja.
Sababu  kubwa ni kwamba  majengo marefu na milima/mabonde huzuia hewa ya kutosha ,mwanga na huweka kivuli (giza) kwenye nyumba.
Habari njema ni kuwa kiwanja kilicho na milima ama majengo marefu upande wa kusini na upande wa magharibi husaidia kuzuia miale mikali ya mwanga.
10.  Epuka kiwanja kilicho na  nguzo kubwa za umeme kwenye kona ya kaskazini-mashariki.
Sababu kubwa ni kwamba umeme unaopita kwenye nguzo huwa na mawimbi (electrical waves) ambazo huwa na madhara na ukubwa wa nguzo huzuia mwanga na hewa kufikia nyumba itakayojengwa.
11.  Epuka kiwanja chenye nyufa/mipasuko(cracks) na udongo wenye mfinyanzi.
Nyufa kwenye ardhi huwa na uhusiano mkubwa na udongo wa mfinyanzi unaoruhusu maji mengi kutuama.Udongo huu si rafiki kwenye ujenzi na huhitaji gharama kubwa kujenga msingi.

12.  .Epuka kiwanja chenye miti mingi yenye mizizi mirefu na minene
Kama kiwanja unachotaka kujenga  ni kidogo na kina miti mingi yenye mizizi mikubwa na minene inayotambaa,si vema kukinunua kwa sababu mzizi hukua na kusababisha nyufa kwenye msingi na hata kufikia kuta za nyumba
13.  Epuka kiwanja kilichopo kwenye makutano ya barabara kuu hasa makutano yenye kutengeneza herufi T ama Y.
Kiwanja kilichopo kwenye makutano huwa na kelele nyingi, vumbi na wakati Fulani huondoa sitiri(privacy). Makutano yenye kutengeneza herufi T ama Y  kuielekea nyumba (kiwanja) ni rahisi kutokea ajali hasa kwa magari kugongana, watu kugongwa wakati wa kuvuka na pia heleta hofu ya kudhani gari zitagonga nyumba.
nyumba iliyojengwa kwenye kiwanja kilicho kwenye makutano ya barabara


14.  Epuka kiwanja chenye umbo la duara,sambusa ama pembetatu.
Kiwanja cha namna hii kama si kikubwa huongeza ugumu katika kuongeza matumizi na kujenga nyumba yenye ukubwa wa kutosha.Katika imani Fulani viwanja vyenye umbile la duara na pembetatu huhusianishwa na huzuni, umasikini na magonjwa.


Ahsante.
Makala imeandaliwa na Pongu J
+255 717 903089, +255 765046644



No comments: